MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Profesa Idris Mshoro |
Profesa Mshoro anasema nchi inakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa mipango miji na vijiji, upangaji wa nyumba na miundombinu, uthamanishi wa ardhi na mali, upimaji ardhi na umilikishaji wa ardhi kwa ujumla. Mfano, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya tathmini ya shughuli za Mipango Miji Tanzania ya Desemba 2014 inaainisha kwamba miji 96, kati ya miji 148 iliyokaguliwa yaani asilimia 65 haikuwa na mpango kabambe wa kuendeleza miji hiyo tangu ilipoanzishwa.
Ili kukabiliana na changamoto hizo Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimetayarisha wataalamu katika maeneo hayo ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa na kumalizwa. Profesa, Mshoro anasema katika mahafali ya tisa ya chuo hicho wamewatunuku wahitimu 937 shahada mbalimbali na kuwataka kuzitumia vyema katika kuendeleza sekta ya ardhi. Waliotunukiwa shahada hizo ni pamoja na wahitimu 880 wa shahada ya kwanza, wahitimu 48 wa stashahada na watano wa shahada za uzamili na uzamivu.
Profesa Mshoro anasema chuo hicho kimepata maendeleo makubwa ukilinganisha na mwaka 2010/11 kilipotoa wahitimu wa kwanza kama chuo kikuu kinachojitegemea, ambapo jumla ya wahitimu walikuwa 323. “Kwa kulinganisha wahitimu 323 wa mwaka 2010/2011 na wahitimu 937 wa mwaka kuna ongezeko la asilimia 190 kwa wahitimu wote….haya ni mafanikio makubwa kwa chuo chetu,” anasema Profesa Mshoro.
Anasema mwaka 2010/11 wahitimu wa kike walikuwa 51 ukilinganisha na 321 sasa, ikiwa in ongezeko la asilimia 529 ndani ya miaka mitano. Aidha, katika muda huo wa miaka mitano (2010 -2015), chuo kimeingiza kwenye soko la ajira jumla ya wahitimu 3,783 wenye shahada mbalimbali, ikilinganishwa na vijana 2,315 waliohitimu ndani ya miaka yote 10 ya uhai wa chuo wakati kilipokuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yaani UCLAS.
Anafafanua kuwa kati ya mwaka 1996-2006 chuo hicho kilikuwa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Chuo hakina budi kujipongeza kwa mafanikio haya makubwa na yanayoongezeka mwaka hadi mwaka. Aidha, ni wajibu wetu pia kuwapongeza wadau wengine waliokisaidia chuo hiki kufikia hapa kilipo sasa,” anasema Profesa Mshoro. Ongezeko la idadi ya wahitimu limetokana na ukweli kwamba Chuo Kikuu Ardhi katika uhai wake wa miaka minane sasa kama chuo kikuu kinachojitegemea, kimeongeza kwa kiasi kikubwa udahili wa wanafunzi.
Mwaka wa mwisho wa UCLAS (2006/2007) chuo kilikuwa na jumla ya wanafunzi 1,351 lakini wameongezeka na sasa kina wanafunzi 4,221. Profesa Mshoro anaishukuru serikali kwa kuwawezesha vijana wa shahada ya kwanza kwa kupitia mikopo inayotolewa hivi sasa kwa wanafunzi wengi kwa kuwa bila mikopo hiyo, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo ya Elimu ya Juu isingekuwa kama ilivyo hivi sasa.
“Tunawapongeza pia Bodi ya Mikopo, kwani ufanisi wa utoaji mikopo hiyo nao umeongezeka mwaka hadi mwaka. Tunaishukuru pia Serikali kwa fedha na misaada mbalimbali iliyofanikisha chuo kudahili idadi hiyo ya wanafunzi,” anasema Mshoro.
Hata hivyo alisema idadi ya vijana wenye sifa wanaoomba kujiunga na programu mbalimbali za Chuo Kikuu Ardhi ni kubwa mno kuliko uwezo wa chuo, na hivyo kufanya wengine kukosa nafasi ambapo kulingana na takwimu za udahili wa pamoja zilizotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu kwa udahili wa mwaka 2014/15, walioomba kujiunga na programu mbalimbali za shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Ardhi walikuwa ni 13,742 wakati chuo kina uwezo wa kudahili wanafunzi wapya 1,245 tu kwa mwaka.
“Ni dhahiri kwamba tunahitaji kuongeza uwezo wetu wa kudahili na kuboresha mazingira, hasa katika programu zenye soko kubwa. Kwa kuwa pia wataalamu wetu wanafanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika maeneo yote yaliyotajwa, ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita, zaidi ya miradi 80 mbalimbali zilikuwa zinaendelea katika maeneo hayo,” anasema Mshoro.
Anasema kwa kuwa bado kuna changamoto nyingi za maendeleo ya nchi zinazohitaji utafiti wa majibu ya kitaalamu, tunahitaji pia kuongeza uwezo wetu wa kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa Serikali na jamii kwa kuongeza idadi na sifa za wanataaluma na kuongeza uwezo wa kifedha ili kufanikisha uendeshaji wa programu zetu kwa ubora unaotakiwa.
Anasema katika jitihada hizo, Chuo kimefanikiwa kupata mkopo mwingine toka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ili kuendeleza ujenzi wa jengo la taaluma ambalo litakuwa na kumbi za mihadhara, vyumba vingine vya kufundishia na ofisi za walimu. Chuo hicho kimewasilisha hati ya makubaliano kwa Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya studio za wanafunzi, ambapo pia kimewaomba wadau wengine kutoa ushirikiano kwa chuo hicho.
Pia anasema kwa kushirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo huduma za maktaba na maabara nazo zimeendelea kuboreshwa kwa kuongeza vifaa vya kujifunzia na kufanyia utafiti. Anasema chuo hicho kina mahusiano mbalimbali na vyuo vikuu na taasisi nyingine 62 za ndani na nje ya nchi, yanayohusu uendeshaji wa programu za mafunzo au tafiti za pamoja, na kubadilishana wataalamu na wanafunzi ambazo zimekuwa fursa ya kukuza ubora wa mitaala, utafiti na taaluma kwa ujumla chuoni hapo.
Anasema lengo la chuo ni kuhakikisha wanaendeleza ubora wa shughuli zao kuu, wahitimu wao wanaendelea kukubalika katika soko, na vijana wengi wanaendelea kuvutika kujiunga na chuo hicho na kuongeza nafasi zaidi ya kuwapokea.
“Ni matumaini yetu kuwa Serikali itaendelea kuongeza fursa za ajira kwa wahitimu hawa, ikiwemo uwezekano wa kuwaajiri moja kwa moja, tukitilia maanani upungufu mkubwa wa wataalamu wa aina hii uliopo katika halmashauri zetu na baadhi ya Wizara. Nawahakikishia kuwa wamepikwa vizuri na wameiva,” anasema. Chuo kimekuwa kikiweka mkazo katika mafunzo kwa vitendo.
Aidha, chuo kinaweka msisitizo wa mtangamano wa mafunzo, tafiti na ushauri wa kitaalamu vinavyofanyika, ili kuhakikisha mafunzo yatolewayo yanagusa stadi hai za soko la ajira. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wahadhiri wetu ambao wamekuwa wakitumia uzoefu wanaoupata kupitia utafiti na ushauri katika kufundisha vijana, na hivyo kuwapatia mifano halisi ya majukumu yaliyopo hivi sasa katika fani husika.
Aidha baadhi ya wahadhiri, kwa kiasi kinachokubalika, wamekuwa wakiwashirikisha wanafunzi katika kutekeleza miradi ya ushauri, kama sehemu ya mafunzo, hivyo kuongeza umahiri na weledi wa wahitimu wetu.
kwa hisani ya Habari Leo (HELLEN MLACKY).
0 comments:
Post a Comment